Mshambuliaji wa West Ham United, Michail Antonio amefichua kwamba Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah alitaka kuondoka kipindi cha usajili wa kiangazi huku Al-Ittihad ikionyesha nia ya kumsajili.

Hiyo ilikuwa moja ya klabu kwenye dirisha la usajili la kiangazi lililopita baada ya Liverpool kukataa ofa ya Pauni Milioni 150 iliyotolewa na wababe hao kutoka Saudi Arabia.

Taarifa zilisema timu hiyo ilikuwa tayari kurejea na ofa ya nyingine ya Pauni 200 milioni, lakini Kocha Jurgen Klopp alizuia uhamisho kufanyika kwani hakuwa na nia ya kumuuza.

Hata hivyo, Mshambuliaji wa West Ham, Antonio amesisitiza kwamba Salah mwenye umri wa miaka 31 ambaye angekuwa analipwa Pauni 100 milioni kila mwaka, alitamani kujiunga na Al-Ittihad lakini Liverpool ikamuwekea kiwingu.

“Alikuwa na nia ya kuondoka. Kutokana na heshima kubwa aliyokuwa nayo Liverpool hakutaka kuonyesha dharau. Najua alitaka kuondoka, nina uhakika alikuwa tayari kuondoka Anfield,” alisema Antonio.

Licha ya Saudi Arabia kuwa na pesa nyingi, Antonio alidai Salah alikuwa na maslahi mengine binafsi baada ya kukipiga Anfield kwa miaka sita.

Salah ameifungia Liverpool mabao 188 na anashika nafasi ya tano katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa timu hiyo, huku akiwa ameshinda mataji yote ikiwemo Ligi Mabingwa Ulaya.

Licha ya uhamisho kukwama haikuathiri kiwango cha Salah kwani alifunga mabao mawili na kutoa asisti nne kwenye mechi tano za mwanzo wa msimu huu za Ligi Kuu England.

Kwa mujibu wa taarifa Al-Ittihad inaamini itanasa saini ya Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Misri na inapanga kurudi tena mwakani.

Milioni 150 za GGML kudhamini maonesho ya Madini, Teknolojia
Tumieni fursa kilele cha Mwenge kibiashara - RC Sendiga