Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuwa tayari kwa mabadiliko yenye lengo la kuiboresha sekta ya ardhi.
Silaa amesema hayo hii leo Septemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na watumishi wa Sekta ya Ardhi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na watumishi hao tangu ateulie kuiongoza Wizara hiyo.
Amesema, ‘’tuna kazi kubwa ya kufanya reforms nyingi katika Wizara hii, ambazo zinalenga kumhudumia mtanzania. Mifumo ya ICT, TEHAMA, upimaji wetu, nchi inatakiwa kupimwa na kupangwa ili kupunguza migogoro ya ardhi na Waziri aliyekuja anafanya kazi kubwa ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya ardhi.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi, mabadiliko yanayofanyika yanalenga kutengeneza mazingira ya makazi na ardhi inayosimamiwa na wizara, kuwa katika sura inayoenda kumsaidia Mtanzania wa leo na miaka 50 baadaye.