Kocha Mkuu wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema anataka kubeba Ubingwa wa Europa League na watapambana kufikia malengo hayo kwani wapo kwa ajili ya kushindana msimu huu.

Klopp amesisitiza hatapanga kikosi chenye wachezaji vijana watupu bali atachanganya pia baadhi ya wachezaji wake hatari wa kikosi cha kwanza.

Mashabiki wa Liverpool kabla ya michuano hiyo kuanza waliamini kwamba Klopp atawapumzisha baadhi ya mastaa wao kama Mohamed Salah, Virgil Van Dijk na Dominik Szoboszlai.

Lakini Klopp amesisitiza atawapa pia nafasi wachezaji vijana kama Ben Doak na Jarell Quansah kwani wameanza kumshawishi kutokana na juhudi zao mazoezini.

Pia wachezaji waliopoteza nafasi ya kudumu kikosi cha kwanza kama Harvey Elliott, Joe Gomez na Caoimhin Kelleher wanaamini watapewa nafasi ya kucheza kwenye michuano hiyo.

“Tupo hapa kwa ajili ya kushindana sio kuwapa nafasi wachezaji. Najua tunapewa nafasi kubwa na tumeichukulia kwa uzito wake na tunataka kushinda.” alisema Klopp

Mara ya mwisho Liverpool kucheza Europa ilikuwa kwenye fainali dhidi ya Sevilla mwaka 2016 hata hivyo ikapoteza mchezo.

Lakini Klopp alikiri michuano ilikuwa migumu kwa Liverpool mwaka huo: “Nakumbuka tulisafiri umbali mrefu, timu yetu ilikuwa bado lakini matokeo mabovu yalitusaidia sana, tukaja kucheza Uswiz kwenye uwanja mbovu mambo yalikuwa mengi.

“Hatukuwa tayari kipindi hicho lakini timu iliimarika na tukaanza kucheza kwa kiwango cha juu.” aliongeza.

JKT Tanzania yaipeleka Kagera Sugar Shinyanga
Julio: Young Africans ni timu bora