Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho amekiri kufurahishwa na mwenendo wa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbiji Jose Luis Miquissone, ambaye alirejea klabuni hapo mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuvunja mkataba wake na Al Ahly ya Misri.

Miquissone amekuwa na wakati mgumu wa kurejea katika kiwango chake kama ilivyozoeleka tangu aliporejea klabuni hapo, lakini Kocha Mkuu Robertinho anaamini Kiungo huyo atafanikiwa kurudi kwenye ubora, kufuatia nafasi anayompa kikosini kwake.

Miquissone alitumika kwa dakika 90 za mchezo wa juzi Alhamis (Septemba 21) dhidi ya Coastal Union na kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema anamuona yule fundi anayesubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo kwani ameanza kurudi kwenye ubora wake.

Katika mchezo huo wa juzi, Miquissone alisabalbisha bao la tatu lililofungwa kwa penalti baada ya kufanyiwa madhambi ndani ya boksi lakini alifanya kitendo kilichowakosha mashabiki kwa kumpa Baleke aliyekuwa amefunga mabao mawili akamilishe hat-trick’ yake, na kujinyima fursa ya kuandika bao lake la kwanza la zote 90 bila kuchoka.

“Awali alikuwa hawezi kufanya hivi, lakini tumemuona akizidi kuwa bora na kutochoka, hili ndilo tunalotaka kwani tukiwa wote kwenye ubora inatusaidia,” amesema Robertinho ambaye alikuwa anasema mara kwa mara mchezaji huyo hakuwa fiti kwa sababu alichelewa kujiunga na wenzake katika pre-season.

Robertinho amesema anafurahi kuona wachezaji wake wakizidi kuimarika kadri siku zinavyokwenda mbele na kwamba timu inakua kwa pamoja, jambo ambalo anajivunia kwani litamsaidia katika siku zijazo.

“Timu yangu ina makundi mawili, lakini yote yapo sawa kwa kulingana kwa sasa jambo ambalo linanipa nguvu katika kila mchezo unaokuja. Viwango vya wachezaji vinazidi kuimarika, hii inafurahisha.”

Kuhusu mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia waliotoka nao 2-2, amesema wanajiandaa vyema.

Simba SC itakuwa mwenyeji katika mchezo huo utakaopigwa Jumapili (Oktoba Mosi) katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es salaam.

Joao Felix: Sikuwahi kufurahia maisha Madrid
Mkutano Polisi wa kike Duniani IAWP wafungwa rasmi