Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi, amewaambia washambuliaji wake kwamba, anataka kuona wanahakikisha wanafunga mabao zaidi katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ili kujiweka mazingira ya kufuzu kwa kishindo.

Gamondi ametoa kauli hiyo, Young Africans ikiwa na matumaini ya kufuzu hatua yą makundi ya michuano hiyo kufuatia ushindi wa mabao 0-2 ilioupata ugenini katika mchezo wa kwanza uliopigwa Kigali, Rwanda.

Jumamosi (Setemba 30), Young Africans itakuwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex, Dar, kurudiana na Al Merrikh ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gamondi amesema kikosi chake kimeanza mazoezi, huku akihitaji safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Kennedy Musonda, Hafiz Konkoni na Clement Mzize kuongeza umakini katika kuhakikisha inatumia kila nafasi watakayoipata katika mchezo huo.

Gamondi amesisitiza kuwa, wanatambua kama wana mchezo mgumu mbele yao, hivyo wanahitaji mabao mengi kuhakikisha wanaweka rekodi katika michuano hiyo.

“Tunahitaji mabao mengi zaidi katika mchezo ujao maana kila timu inahitaji ushindi katika hatua hii ili kufuzu hatua ya makundi.

“Wenzetu walipoteza mchezo wa kwanza, naamini wanaporudi uwanjani tena watarudi kivingine kuhakikisha wanapata ushindi, tunatakiwa kwenda kupambana ili kupata matokeo makubwa kwa kuhakikisha tunafunga mabao mengi,” amesema Gamondi.

Ikumbukwe kuwa, hatua ya kwanza katika michuano hiyo msimu huu, Young Africans iliiondosha ASAS ya Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1.

Msimu uliopita timu hiyo ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kushika nafasi ya pili.

Simamieni matumizi sahihi ya fedha za Serikali - Dkt. Biteko
Kakolanya: Tutatinga Makundi Shirikisho