Maafisa Ununuzi wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo wakati wa ununuzi wa vifaa na vitendea kazi vyenye kemikali zilizowekewa ukomo wa matumizi, ili kuzuia athari uharibifu wa mazingira na kulinda afya za binadamu.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Abdalllah Mitawi wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa Maafisa Ununuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.
Amesema, asilimia kubwa ya bajeti ya Serikali imeelekezwa katika eneo la ununuzi wa vifaa na vitendea kazi mbalimbali katika ofisi za umma, hivyo ni wajibu wa maafisa manunuzi kuhakikisha wanazingatia miongozo iliyoainishwa, ili kuepusha hasara kwa serikali na kulinda afya kwa binadamu na mazingira.
“Maofisi yote ya umma tunatumia viyoyozi na majokozi kama sehemu ya kupata hewa safi…Maafisa ununuzi ndio mnahusika moja kwa moja katika ununuzi wa vitendea kazi hivi. Tunapaswa kufahamu kuwa kunaaina fulani ya kemikali zilizopo katika vitendea kazi hivi zina athari kwa mazingira yetu….kupitia mafunzo haya mtaweza kufahamishwa,” amesema Mitawi.
Aidha ameongeza kuwa, Tanzania iliridhia mkataba huo mwaka 1993, nchi zote 197 zimekubaliana kutotumia kemikali zilizodhibitiwa kupitia ili kulinda Tabaka la ozoni kwa kuwa hatua hiyo itasaidia juhudi za ulimwengu kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto, ukame na vifo vya binadamu, wanyama na mifugo.