Mshambuliaji Jadon Sancho ameombwa na wachezaji wenzake kwenye klabu hiyo kumuomba radhi kocha wao, Erik ten Hag.

Sancho amewekwa kando kufanya mazoezi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kufuatia mgogoro wake na kocha Ten Hag uliotokana na nyota huyo wa kimataifa wa England kutupwa benchi kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Arsenal ambapo United ilinyukwa mabao 3-1.

Mzozo huo umedumu kwa majuma matatu na wachezaji wenzake wakiongozwa na Marcus Rashford, Luke Shaw na Harry Maguire, wameingilia kati kutatua mgogoro huo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani kwenye klabu hiyo, Sancho ameambiwa na wachezaji wenzake wa England kumuomba radhi Ten Hag ili kuokoa kibarua chake kwenye klabu hiyo.

Sancho hakuchaguliwa kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Brighton, Bayern Munich na Burnley huku akiendelea kuwekwa pembeni.

Pia amewekwa pembeni kwenye maeneo yanayowahusu wachezaji wa kikosi cha kwanza cha United kama kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, sehemu ya kula chakula kwa sasa anafanya mazoezi peke yake.

Chama cha Wachezaji wa kulipwa (PFA) pia kimejitolea kutatua ugomvi huo wa Sancho na Ten Hag.

Nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmund yuko tayari kuondoka kwenye klabu hiyo wakati wa dirisha dogo lakini bado ana mkataba na Manchester United mpaka mwaka 2026.

Taaluma ya Madini: GGML yawanoa Wanafunzi Nyankumbu
Henock Inonga kurudi mazoezini Simba SC