Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema takriban watu 186,000 wamewasili Ulaya kupitia bahari ya Mediterania mwaka huu hali ambayo inazidi kuyatikisa Mataifa ulimwenguni.

Mkurugenzi wa ofisi ya UNHCR mjini New York Ruven Menikdiwela ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba watu 130,000 wamesajili nchini Italia idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Menikdiwela ameeleza kuwa, zaidi ya watu 2,500 hawajulikani waliko au wamekufa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi Septemba 24 ambapo hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM lilitoa takwimu zilizoonyesha kuwa, zaidi ya watu 2,700 hawajulikani waliko au wamekufa.

Ongezeko la idadi ya wahamiaji tayari limesababisha mivutano ndani ya Umoja wa Ulaya juu ya hatua za kudhibiti wimbi la wahamiaji na Viongozi wa nchi tisa za Mediterania na kusini mwa Ulaya, akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, wanakutana leo nchini Malta kwa mazungumzo yatakayojikita juu ya suala la wahamiaji.

@Source DW.

Tanzania, Saudi Arabia zajadili kukuza Utalii Nchini
Mlipuko wa Bomu la kutegwa wauwa sita Sokoni