Beki wa kati wa Tabora United Kelvin Kingu Pemba atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi miwili baada ya kuvunjika mshipa wa mguu wa kushoto wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Big Stars.

Daktari wa timu hiyo, Abel Shindika amesema baada ya nyota huyo kutoka DR Congo kufanyiwa vipimo vya kina imegundulika jeraha lake lilikuwa kubwa jambo ambalo limekuwa pigo kwenye kikosi hicho.

“Awali ilionekana jeraha lake ni la kawaidia lakini tumegundua lina ukubwa wake ndio maana tumempa mapumziko ya zaidi ya mwezi mmoja na wiki tatu kwa lengo la kuhakikisha anarejea uwanjani akiwa imara zaidi,” amesema.

Kwa upande wa kocha mkuu wa timu hiyo, Goran Kopunovic amesema ni pigo kumkosa nyota huyo kwa kipindi kirefu ingawa usajili uliofanyika msimu huu ndani ya kikosi hicho unampa matumaini kutokana na wingi wa wachezaji.

“Kwa michezo iliyopo mbeleni ni jambo la kuumiza sana unapokosa mchezaji muhimu kikosini lakini ndio mpira wa miguu ulivyo, kwetu ni pengo ila tunashukuru tuna wachezaji wengi ambao wanaweza kucheza nafasi hiyo.”

Pemba amejiunga na klabu hiyo msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuachana na Mbabane Swallows ya Eswatini.

Robertinho: Nimesikia malalamiko ya Mashabiki
Mason Greenwood habari nyingine Hispania