Imeelezwa kuwa, Shirikisho la soka la nchini Italia (FIGC) linafikiria kumshitaki aliyekuwa Kocha Mkuu wa Timu ya taifa hilo Roberto Mancini kutokana na kuacha kazi ghafla, imeelezwa.

Mancini mwenye umri wa miaka 58, aliacha kazi ya kukinoa kikosi cha The Azzurri, Agosti l3 mwaka huu baada ya kuifundisha timu hiyo kwa miaka mitano.

Majuma mawili baadae, alikubali dili la miaka minne kwenda kuwa kocha wa Saudi Arabia, na kwenye ajira hiyo mpya, Mancini ameripotiwa kwamba analipwa mshahara wa Pauni 21.5 milioni kwa mwaka baada ya makato ya kodi.

Na sasa rais wa FIGC, Gabriele Gravina amesema kwamba wanafikiria kupata ushauri wa kisheria juu ya jambo hilo, huku wakitazama kuona kama wanaweza kumshtaki kocha huyo kwa kuacha kazi ghafla.

Saudi Arabia ilikuwa ikinolewa na Herve Renard kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika nchini Qatar, lakini Mfaransa huyo alimwaga manyanga Machi mwaka huu na kwenda kuifundisha timu ya taifa ya soka ya wanawake ya huko kwao Ufaransa.

Mancini alishaiongoza Saudi Arabia kwenye mechi mbili, ambapo ya kwanza ilikuwa ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Costa Rica, kisha ikapata ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Korea Kusini.

Mechi hizo zote zilifanyika kwenye Uwanja wa St James’ Park unaomilikiwa na Newcastle United ya England, lakini Mancini hakuzungumza na vyombo vya habari baada ya mechi. Huko Italia nafasi yake ilichukuliwa na kocha Luciano Spalletti.

Mancini aliongoza Italia kushinda ubingwa wa Euro 2020 na iliweka rekodi ya kucheza mechi 37 bila ya kupoteza.

Kwikwi Ligi Kuu yamtibua Kocha Mtibwa Sugar
Kocha JKT Tanzania alia na wachezaji wake