Kocha wa muda wa Singida Fountain Gate, Ramadhani Nswanzurimo amesema sababu ya timu yao kupoteza mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC, ni wachezaji wake kupoteza umakini.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Al Salaam, Cairo wenyeji Future ilishinda mabao 4-1 nakufanya matokeo ya jumla kuwa zaidi ya mabao mawili, baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Dar es salaam, Singida FG kushinda bao 1-0.

Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema kasi ya kipindi cha pili waliyoingia nayo wapinzani wao ilisababisha wachezaji wake kufanya makosa mengi ambayo yaliwanufaisha wapinzani wao nakujikuta wanapoteza mchezo.

“Tulikuwa na matarajio makubwa ya kutinga makundi baada ya kipindi cha kwanza kumalizika tukiwa sare ya bao 1-1, lakini kipindi cha pili wachezaji walishindwa kutekeleza kile ambacho tulikubaliana, Future walitupa presha kubwa iliyosababisha wachezaji wetu kufanya makosa na kuruhusu mabao matatu,” amesema Nswanzurimo.

Kocha huyo amesema kutokuwa na uzoefu wa kutosha nako kumechangia washindwe kusonga mbele kwenye michuano hiyo ingawa anafurahi kuwa pamoja na kutolewa lakini kuna kitu wamekipata kwenye michuano hiyo.

Amesema wamerudi nyumbani kuendelea na Ligi Kuu na mashindano ya Kombe la FA, lengo lao likiwa ni kufanya vizuri ili msimu ujao warudi tena kwenye michuano hiyo ambayo anaamini watafika mbali.

Katika mchezo huo, Singida FG ilihitaji suluhu, sare au ushindi wowote au hata kufungwa mabao 2-1 ili kutinga hatua ya makundi lakini ilishindwa kuhimili presha ya wapinzani wao Future ambao ushindi huo umewavusha katika hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo tangu kuanza kushiriki michuano hiyo.

Yamal kung'oka Barcelona kwa masharti magumu
Waliogundua chanjo ya Uviko-19 Washinda Tuzo ya Nobel