Wakati Kagera Sugar ikipania kuutumia vyema uwanja wa nyumbani, Kocha Mkuu wa Namungo FC, Cedric Kaze ameweka wazi kuwa, amekiandaa vyema kikosi chake kushinda mchezo wa leo Jumatano (Oktoba 04).

Kagera Sugar itachuana na Namungo FC katika mechi ya raundi ya tano ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayopigwa katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amesema kuwa, amekiandaa vizuri kikosi chake kuikabili Namungo FC na lengo lao ni kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

Mexime amesema timu yake ina wachezaji wenye viwango vya juu, hivyo hana sababu ya kuwahofia Namungo FC.

“Tumejipanga Kuhakikisha tunashinda mchezo, wachezaji wangu wote wapo fiti na naamini tutautumia vizuri uwanja wa nyumbani,” amesema.

Kwa upande wa Kocha Kaze amesema kikosi chake kipo imara, kwani ameinoa vyema safu yake ya ushambuliaji kuhakikisha haipotezi nafasi za wazi.

Amesema lengo la kikosi hicho ni kuvuna pointi tatu katika mechi hiyo kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Najua utakuwa mchezo mgumu kwa sababu wapinzani wetu pia wapo imara, lakini tayari nimerekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza katika mchezo uliopita hasa katika safu ya ushambuliaji, naamini tutaondoka na ushindi wa mabao mengi.” amesema.

Katika msimamo wa ligi hiyo msimu huu, Kagera Sugar inashika nafasi ya tisa kwa kufikisha pointi nne wakati Namungo FC ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi mbili.

Arsenal wamuita mezani Ben White
Makali mapya bei za Mafuta zikizidi kupaa