Uongozi wa Klabu ya Arsenal umeanza mazungumzo rasmi na beki wake Ben White, ili kufanikisha mpango wa kumsainisha mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Kaskazini mwa jijini London.

Katika mazungumzo hayo, Uongozi wa Arsenal una uhakika kuwa beki huyo kutoka England mwenye umri wa miaka 25, atakubaliana na mipango ya klabu, na kukubali kusaini mkataba mpya.

White amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha The Gunners tangu alivyotua mwaka 2021 akitokea Brighton ya nchini humo.

Tovuti ya michezo ya Daily Mail mwezi uliopita iliripoti kuwa, Arsenal ilikuwa katika maandalizi kuanza mazungumzo kumwongeza mkataba nyota huyo.

Tovuti hiyo mapema juma hili ilieleza kuwa, tayari Arsenal na beki huyo wameshaanza mazungumzo kuona uwezekano wa kumwongeza mkataba.

Pamoja na White kubakisha miaka mitatu katika mkataba wake wa sasa, Arsenal inahitaji kukamilisha dili hilo kwa haraka ili kuendelea kupata huduma ya beki huyo kwa muda mrefu zaidi.

Mchezaji huyo ambaye ana uwezo wa kucheza kama beki wa kati na pembeni, hivi sasa analipwa mshahara wa Pauni 120,000 kwa juma.

Ikiwa atasaini mkataba mpya, Daily Mail imeripoti kuwa, mshahara wa beki huyo utaongezeka.

Beki huyo, amekuwa na mfululizo wa kiwango bora katika kikosi cha Arsenal kinachonolewa na kocha Mikel Arteta.

Tayari Arsenal imewashawaongezea mikataba baadhi ya wachezaji wake ambao wanafanya vyema katika kikosi hicho.

Miongoni mwa waliosaini mikataba mipya hadi sasa klabuni hapo ni Bukayo Saka, Martin Odegaard, Gabriel Martinelli, William Saliba na Reis Nelson.

Minziro atangaza hatari uwanja wa Sokoine
Kaze, Mexime watambiana Ligi Kuu