Bilionea Sir Jim Ratcliffe anafikiria kuachana na mpango wake wa kuinunua Klabu ya Manchester United kwa sababu anatakiwa kuchukua hisa chache jambo ambalo litaiacha familia ya Glazer kuwa na udhibiti mkubwa wa klabu hiyo.
Katika hali ya mshtuko ambayo bila shaka itachochea hasira miongoni mwa mashabiki wengi wa United, bilionea huyo wa kemikali za petroli anatafakari juu ya mabadiliko ya mbinu katika jaribio la kuvunja mkwamo kwenye kile ambacho kimekuwa ni mchakato wa kuchosha ambao sasa unakaribia mwezi wake wa kumi.
Msemaji wa Ratcliffe alikataa kutoa maoni yoyote, lakini inafahamika kuwa moja ya chaguzi zilizokuwa zinaangaliwa ni ununuzi wa asilimia 25 ya hisa za United.
Hiyo inaweza kuleta kiasi cha karibu Pauni Bilioni 1.5 kwa familia ya Glazers, ambao walilipa Pauni Milioni 800 mwaka 2005 kuinunua klabu hiyo.
Bei ambayo familia ya Glazer inaitaka kwa sasa ili kuiuza klabu hiyo ni Pauni Bilioni sita, lakini bado imeonesha nia ya kutotaka kuiuza kwa hisa zote 100.
Mashabiki na wafuasi wa Man United tayari wameandamana dhidi ya wamiliki wa sasa na wametaka iuzwe jumla.
Kwa mujibu wa Sky News, ambao walitoa habari za maendeleo ambayo vyanzo vilithibitisha baadae kwa Mail Sport, ofa kama hiyo inamfanya Ratclife kuwa na udhibiti mdogo kwa timu hiyo.
Mpinzani mkuu wa Ratcliffe, Sheikh Jassim Bin Hamad Al Thani, aliwasilisha ombi lake la mwisho la kuinunua moja kwa moja klabu mwezi Mei.
Mail Sport inaelewa kuwa raia huyo wa Qatar bado amejitolea kuitwaa klabu hiyo kwa asilimia 100.