Klabu ya Liverpool imeiomba Kamati Iya Waamuzi (PGMOL) sauti za majadiliano ya marefa waliochezesha mchezo kati yao na Tottenham ambao walifungwa mabao 2-1.
Waamuzi wa Teknolojia ya Video (VAR) walilikataa bao la timu hiyo lililofungwa na mshambuliaji Luis Diaz kwa kigezo cha mfungaji alikuwa ameotea.
Kamati hiyo ya waamuzi ilisema yalikuwa makosa ya kibinadamu yaliyofanywa na waamuzi wa mechi hiyo kulikataa bao hilo la Liverpool.
Jumapili (Oktoba Mosi), Liverpool ilitoa taarifa maelezo hayo hayakubaliki na kwamba heshima ya mchezo wa soka imeharibiwa.
Klabu hiyo iliomba marejeo ya tukio hilo kwa uwazi na kuongeza kuwa wataangalia hatua mbalimbali za kuchukua yenye lengo la kutatua suala hilo.
Darren England, aliyekuwa akisimamia VAR kwenye mechi hiyo na msaidizi wake Dan Cook waliondolewa kwenye majukumu hayo kufuatia makosa hayo.
Kamati ya Waamuzi ilibaini maofisa wa VAR walishindwa kutoa maamuzi sahihi baada ya Diaz kufunga bao dakika ya 34 na ku- kataliwa.
Wakati bao hilo linakataliwa matokeo ya mchezo huo yalikuwa 0-0 huku Liverpool walikuwa wakicheza pungufu kufuatia kadi nyekundu ya Curtis Jones.