Bosi wa mpira, Paul Mitchell ambaye amekuwa maarufu kwa kuibua vipaji vya wanasoka wengi Barani Ulaya, ameng’oka kwenye wadhifa wake wa mkurugenzi wa michezo huko AS Monaco.
Mitchell aliwahi kufanya kazi Southampton na Tottenham Hotspur na sasa anahusishwa na mpango wa kurudi kwenye Ligi Kuu England baada ya kuachana na klabu ya Ligue 1.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano, AS Monaco imeamua kumpa kazi Thiago Scuro.
Kuhusu Mitchell aliwahi kuhusishwa na Manchester United na mashabiki wa miamba hiyo ya Old Trafford wanaamnini atanaswa akapige mzigo kwenye timu yao.
Shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa X: “Ajiunge Manchester United, wamiliki waje wapya pia.”
Mwingine aliandika: “Ni bora kuliko mkurugenzi wa soka wa sasa wa Man United (John) Murtough. Kwanini tusimchukue haraka.” Na shabiki wa tatu alisema: “Hapa Man United tunahitaji mtu wa aina hii.”
Shabiki mwingine aliposti: “Manchester United imwaajiri” na mwingine alisema: “Mchukueni Paul Mitchell.”
Mitchell aliwahi kucheza Manchester City na Wigan utotoni, lakini alistaafu akiwa na miaka 27 mwaka 2009 kutokana na kuwa majeruhi na hivyo kuingia kwenye kazi ya ukurugenzi.
Akiwa MK Dons alimsajili Dele Alli na alipokwenda Southampton alinasa saini za mastaa Maya Yoshida, Nathaniel Clyne, Sadio Mane, Dusan Tadic na Graziano Pelle.
Alipokwenda Spurs mwaka 2014 aliwanasa Kieran Trippier, Toby Alderweireld, Son Heung-Min na Dele Alli tena, wakati RB Leipzig aliwasajili Dani Olmo, Christopher Nkunku, Ademola Lookman, Patrik Schick, Dayot Upamecano na Matheus Cunha na kwenye kikosi cha Monaco aliwasajili wakali kama Axel Disasi na Breel Embolo.