Timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma, imepongezwa kwa kuendelea kufanya vizuri katika suala la uchangiaji damu hadi kuvuka lengo la asilimia 100 lililowekwa na kufikia asilimia 110 kwa sasa.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah ametoa takwimu hizo jijini Dodoma wakati wa zoezi la uchangiaji damu lililoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Amesema, suala la uchangiaji damu ni la muhimu na msingi kwani ni muhimu kuhakikisha damu na mazao ya damu yanakuwepo kwa wakati wote katika Vituo vya Afya kwani kunaweza kuwa na wataalam wakafanya kila kitu lakini kama hakuna damu msaada hautofanya kitu chochote.

“Kuchangia damu ni jambo la msingi, hali ya uhitaji wa damu ni kubwa hasa kwa mikoa yenye idadi kubwa ya watu na tunatamani angalau kila mkoa uwe na asilimia 85 mpaka 90, tunaipongeza Timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma kwa kuvuka lengo lililowekwa,” alisema Bi. Ziada.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, amewakaribisha wananchi kuchangia damu ili kuwa na damu ya kutosha katika ghala za kutunzia damu kwa ajili ya kusaidia wenye uhitaji wakiwemo wagonjwa waliopata ajali, wajawazito na watoto wenye upungufu wa damu.

Granit Xhaka: Mnamsingizia, niliamua mwenyewe
Jafo aipongeza NEMC usimamizi sheria ya Mazingira