Asasi za kiraia zinazotetea haki za Wanawake Zanzibar, kwa pamoja zitazindua waraka wa mapendekezo ya sheria unaolenga kuwawezesha Wanawake wengi kupata haki ya kushika nafasi za Uongozi katika ngazi za maamuzi.
Uzinduzi huo, unatarajia kufanyika Oktoba 5, 2023 mjini Unguja ambao utawahusisha washiriki 80 kutoka Taasisi za Serikali, zisizo za Kiserikali na Waandishi wa Habari ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar – TAMWA-ZNZ.
Nyingine ni Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar – ZAFELA, Jumuiya ya Utetezi wa Kimazingira na Jinsia Pemba – PEGAO na Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar – JUWAUZA huku uzinduzi huo ukija kufuatia kukamilika kwa mchakato wa kupitia sheria, sera na katiba za vyama vya siasa.
Mchakato huo, pia uliwashirikisha wadau mbali mbali na kuona mapungufu mengi yakiwemo kutozingatiwa usawa wa kijinsia kwa kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na azimio la 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotolewa Oktoba 31, 2000 lisemalo “Kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi kunakuza demokrasia ya nchi, uchumi, amani na utulivu kwa muda mrefu.”
Aidha, Mkataba wa kimataifa unaopinga aina zote za udhalilishaji dhidi ya wanawake – CEDAW, wa 1979 katika kifungu cha 7, unasisitiza kuwa na haki sawa baina ya mwanamke na mwanamme katika uchaguzi na mchakato mzima wa upigaji kura na kuchaguliwa kushika madaraka.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina idadi ya watu wapatao kubwa kuliko wanaume 1,889,773 inaonyesha kuwa idadi ya wanawake ni 974,281 ambayo ni kubwa kuliko wanaume.
Hata hivyo, ilibainika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kuwa jumla ya wanawake 294,237 sawa na asilimia 51 waliandikishwa kama wapiga kura ikilinganishwa na wanaume 272,115 ambao ni sawa na asilimin 49.