Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kipindi cha kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 2, 2023 limewakamata watuhumiwa 22 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo mauaji, uvunjaji, kupatikana na nyara za Serikali, kupatikana na Bunduki bila kibali, Dawa za kulevya na watu waliojifanya Maafisa wa Jeshi la Polisi.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoani humo Kamishina Msaidizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga amesema, watuhumiwa hao ni pamoja na Juma Mapunda (47) na Said Wanyika (27) wote wakazi wa Songea Mkoa wa Ruvuma, ambao walijifanya maafisa wa Polisi.
Watu hao, walikamatwa Mji mdogo wa Mbalizi maeneo ya stendi ya Tunduma katika misako iliyoendelea wakijitambulisha hivyo kwa Wananchi kisha kumkamata na kumtapeli Mtu mmoja Meck Frank pesa taslimu Shilingi 700,000 pamoja na simu tatu.
Kamanda Kuzaga amesema, Polisi Mkoa wa Mbeya pia inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bangi kilo 87 na gramu 60, ambao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya wakiwa wanasafirisha na kuuza.
Waliokamatwa ni Blandina Silvester, Mkazi wa Tarafani Mbalizi, Samson Samwel, Bruno Zubery wote wakazi wa Itumbi na Jofrey Omondi raia na Mkazi wa Migori nchini Kenya, ambaye alikamatwa akiwa na Bangi kilo 30 zikiwa zimezungushiwa kwenye mifuko mieusi ya plastick na kuwekwa kwenye begi mbili.
Mtuhumiwa alikuwa anasafirisha bhangi hiyo kwenye gari Basi la abiria lenye namba za usajili T.205 DKG aina ya Scania mali ya Kampuni ya Premier Line akitokea Mwanza kwenda Mbeya.