Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umetoa kauli yake mara baada ya timu yao kupoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu 2023/24, ukisema wamepoteza mechi na sio ubingwa wao wanaoushikilia.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Young Africans, Arafat Haji, akisema hatua ya timu yao kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya hefu FC si kitu kipya, ingawa hawakutarajia matokeo hayo.
Arafat amesema hata msimu uliopita walipoteza mbele ya Ihefu FC kwenye uwanja huo huo, lakini bado wakatwaa ubingwa na pia wakacheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa baada ya matokeo hayo uongozi wao umeyachukua kama changamoto na sasa wanajipanga kuinuka na gia kubwa kurudi kwenye ramani ya ushindi kupitia mchezo wao ujao dhidi ya Geita Gold, utakaopigwa kesho Jumamosi (Oktoba 07), Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
“Hayakuwa matokeo ambayo tuliyatarajia lakini kuna wakati kwenye soka unatakiwa kupokea hali hiii, tumepoteza mchezo wa kwanza msimu huu, haina maana kwamba tumepoteza ligi nzima.
“Tunarudi kujipanga, mashabiki wetu wasitoke mchezoni kwa matokeo haya, jambo zuri yamekuja mapema, yanatupa nafasi ya kujipanga ndani na nje ya uwanja ili mchezo ujao turudi kwenye njia ya ushindi kama kawaida yetu,” amesema Arafat.