Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Angel Gamondi amekiri kwamba ana wasiwasi na viwanja vya mikoani na vimechangia timu yake kutocheza vyema na kupoteza mchezo uliopita dhidi ya lhefu FC huku akiwatahadharisha waamuzi kutovumilia wachezaji wanaopoteza muda na kuharibu ladha ya mchezo.

Gamondi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa (Oktoba 6) jijini Mwanza wakati akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi (Oktoba 07) dhidi ya Geita Gold, utakaopigwa kuanzia saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba.

“Maandalizi kwa upande wetu siyo mazuri sana kutokana na ratiba lakini sisi ni wataalamu na ligi kuna muda inakuwa na ratiba ngumu lazima kuwa tayari. Leo tutakuwa na mazoezi jioni, ambayo yatatusaidia kuona hali ya wachezaji kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya Geita Gold”

“Kiukweli nina hofu na Uwanja, hatujafika kuuona lakini tutakwenda baadae jioni, pia maamuzi ya waamuzi kwani baadhi ya timu zinapoteza muda na kuharibu kabisa ladha ya mchezo’ amesema Kocha huyo na kuongeza,

“Kama ilivyokuwa mchezo uliopita ambapo tulishindwa kucheza tulivyozoea kucheza pale Taifa na Chamazi kwa hiyo nina wasiwasi na uwanja lakini hatuogopi, japokuwa hatutakuwa na possession tuliyoizoea na wachezaji watahitaji kufikiria sana ili kuendana na uwanja na kucheza vizuri

“Silalamiki lakini waamuzi wanahitaji kuulinda mpira, watu wafurahie tulinde timu inayohitaji kucheza mpira na siyo kupoteza muda,”

“Tumepoteza mchezo uliopita dhidi ya Ihefu, lakini mashabiki wameendelea kuwa pamoja nasi na kutupa sapoti kama vile bado hatujapoteza mchezo wowote ni kazi yetu sasa kuhakikisha kwenye mchezo wa kesho tunajitoa kwa nguvu zote kuhakikisha tunapata ushindi”  amesema Gamondi.

Kocha Azam FC afichua siri ya Msenegali
Bangala, Dube kuikosa Coastal Union