Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi, amesema hataki kuongea lolote kuhusu mechi za hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa BArani Afrika, badala yake ameweka wazi kuwa akili yake ipo kwenye mchezo unaofuata wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Oktoba 25, mwaka huu.
Amesema baada ya kufanikiwa kupata alama tatu ugenini dhidi ya Geita Gold FC juzi Jumamosi (Oktoba 07), nguvu zao wanazielekeza kwenye mechi yao dhidi ya Azam FC, kwani wakati wa kuzungumzia mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, haujafika.
Young Africans inatarajia kutumia mechi hiyo kama maandalizi ya michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itaanzia Ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria Novemba 25, mwaka huu.
Gamondi amesema baada ya kuvuna alama tatu mbele ya Geita Gold FC sasa wanarejea uwanja wa mazoezi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na kujiandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Azam FC.
Amesema muda huu hafikirii mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zaidi ya kufanyia kazi kikosi chake kwa ajili ya mechi yao ijayo dhidi ya Azam FC ambayo itakuwa ya ushindani kwa sababu ya kila timu kuhitaji matokeo chanya.
“Kwa Sasa tunaangalia mechi iliyopo mbele yetu, tunafanyia kazi mechi baada ya mechi, nimeona kundi letu, lakini kabla ya kukutana na timu hizo tunakibarua kigumu cha kutafuta pointi kwenye ligi ya nyumbani dhidi ya Azam FC.
“Kundi ni gumu, ukiangalia timu zote ni bora kwa sababu ya kuzifahamu, kasoro Medeama sijaijua vizuri, kwa sasa tunaangalia kilicho kuwa mbele yetu,” amesema Gamondi.
Ameongeza kuwa amefurahishwa na kiwango kilichoonesha na wachezaji wake kwa kujua kutumia nafasi walizopata na kufanikiwa kuondoka na alama tatu dhidi ya Geita Gold FC.
Kuhusu kupoteza mechi dhidi ya Ihefu FC, amesema wachezaji walikuwa na fatiki kutokana na wiki moja kucheza mechi tatu na kulazimika kufanya mabadiliko ya kikosi tofauti na mpinzani wao huyo yeye alipata muda mrefu wa kujiandaa.
“Kupoteza mechi moja haina maana tumepoteza malengo yetu, ligi ndio imeanza kuna mechi nyingi mbele yetu na lolote linaweza kutokea, kwa sababu kufungwa na sare ni mambo ya kawaida katika mpira,” amesema kocha huyo.
Kuhusu mchezaji wake, Max Nzengeli, amesema ni mchezaji mzuri na anafanya majukumu yake vizuri kwa kushirikiana na wachezaji wenzake kuipa timu matokeo mazuri.