Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya soka ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite Queens’, Ester Chabruma amewapongeza wachezaji wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Djibouti Uwanja wa Azam Complex juzi Jumapili (Oktoba 08).

Chabrumna, nyota wa zamani wa Twiga Stars amesema amefurahishwa na ushindi huo na sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

“Namshukuru Mungu kwa ushindi na nawapongeza wachezaji kwa kuonesha kiwango kizuri. Ni ushindi mzuri unaotuweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele,” alisema Chabruma aliyejulikana kwa jina la utani la Lunyamila wakati anacheza akifananishwa na nyota wa zamani wa Young Africans na Taifa Stars, Edibily Lunyamila.

Katika mhezo huo ambao haukuwa na kingilio mabao ya Tanzanite yalifungwa na Jamila Mnunduka aliyefunga mawili na mengine yakiwekwa wavuni na Noela Lulhala, Winifred na Yasinta Joseph.

Timu hizo zitarudiana Oktoba 11 Uwanja wa Azam Complex ambapo timu itakayosonga mbele itakutana na Nigeria katika mchezo wa kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Colombia mwakani 2024.

Serikali inasikiliza, kutatua kero za Wananchi - Senyamule
Chama atamani ufungaji bora Ligi Kuu