Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewatoa hofu wamiliki wa shule Binafsi juu ya utekelezaji wa mabadiliko ya sera na mitaala mipya ya elimu 2023 kuwa hayatakuwa ya mkupuo na kwamba itasikiliza maoni na mapendekezo yaliyopo kwenye rasimu ya sera na mitaala na utekelezaji wake utakuwa wa awamu.

Hayo yamebainishwa hii leo Oktoba 10,2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wamiliki wa shule zisizo za Serikali na Wizara na kudai kuwa rasimu ya mitaala imeondoa marudio kwa elimu ya msingi kuwa ni miaka sita, lakini mwanafunzi haruhusiwi kukatisha masomo na ni lazima akae shuleni kwa miaka 10.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

Amesema, “mapendekezo yaliyopo kwenye rasimu elimu ya lazima ni miaka 10 ambayo kwasasa ni miaka saba inajumuisha marudio mengi ambayo inaonekana kuchomoa ule mwaka wa saba ili aendelee na kidato cha kwanza hadi cha nne hapotezi kitu.”

Aidha, Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali imefanya maandalizi katika utekelezaji wa jambo hilo, ikiwamo vitabu vya kiada na ziada na kuandaa Walimu huku akitoa wito kwa wamiliki hao kuwekeza kwenye shule za amali na serikali ipo tayari kushirikiana nao kuwekeza kwenye eneo hilo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga amesema kikao hicho kinalenga kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kuzitatua ili kufanya kazi kwa pamoja na kuleta tija kwa taifa huku Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akisema wana wajibu wa kuwaandaa vyema Vijana kwa kushirikiana na taasisi binafsi.

Dkt. Biteko ateta na Wafanyakazi Ubalozi wa Tanzania Uganda
Viongozi wahimizwa kutambua ubunifu wa Vijana