Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Nassoro Hamduni amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatenda haki kwenye mechi za Ligi Kuu Soka Tarnzania Bara.

Hamduni amesema hayo baada ya hivi karibuni kuibuka malalamiko juu ya waamuzi wa mechi za ligi, hasa mechi mbili za Azam dhidi ya Dodoma Jiji na Singida Big Stars dhidi ya Simba SC ambapo inaelezwa mabao ya halali yalikataliwa katika mechi hizo.

“Kwanza nafurahishwa na mwenendo mzuri wa waamuzi, sababu katika mechi hizo za Azam dhidi ya Dodoma na Singida na Simba SC, waamuzi walijitahidi sana japokuwa nao ni binadamu, hauwezi kujua ndani ya mioyo yao kama wanafanya makusudi, bahati mbaya au kwa kutokujua lakini naamini Bodi ya Ligi, TFF na Kamati tumejipanga vizuri kusimamia mchezo huu kwa haki,” amesema Hamduni.

Amesema kama kamati wamekuwa wakisikia kelele juu ya maamuzi wabovu lakini pamoja na hayo wanapaswa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kusubiri ripoti ya wasimamizi wa mechi husika kabla ya kuchukua hatua.

“Tunayasikia malalamiko lakini tunasubiri taarifa rasmi kutoka kamati husika. Ni utaratibu wa kisheria, maana wewe kuona sio jicho la mwisho, katika mpira wa miguu kuna kamati zinahusika, zijiridhishe juu ya taarifa za wanaosimamia mechi na kutupa ushauri kisha kuchukua hatua stahiki,” amesema Hamduni.

Maamuzi ya FIFA yamshangaza Deschamps
Jadon Sancho milango iwazi kuondoka