Lydia mollel – Gairo, Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ametoa wito kwa Viongozi wa Mkoa huo kuhakikisha wanakuwa na uwelewa kuhusu Kilimo, ili kuwaelimisha Wakulima namna sahihi ya kufanya kilimo cha kisasa
Hayo yamejiri katika uzinduzi wa maonesho ya Kilimo na Biashara yaliyofaninyika Wilayani Gairo Mkoani Morogoro, ambayo yamewakusanya wadau mbalimbali wanaounga mkono Kilimo, ikiwemo benki na tasisi za kuelimisha kilimo cha kisasa pamoja na mbegu bora wakilenga kumuwezesha Mwananchi Kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija.
Amesema, hakuna uchawi kwenye kilimo hivyo ukimuona mtu amepata mazao mengi ujue amefuata taratibu za kilimo ikiwemo kuweka mbolea,mbegu bora na ushauri wa wataalam wa Kilimo
Naye mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kubuni vitu tofauti na yeye binafsi anawasapoti wakulima, kwani ameshatoa mashine 120 za kumwagilia mashamba na anatarajia kugawa mashine nyingine 30 kwa Wananchi wa Gairo, ili kuwawezesha kufanya kilimo kwa njia ya kisasa zaidi
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabiri Makame amesema kila mwaka kanda ya mashariki inafanya maenesho ya wakulima nanenane, lakini kutokana na Jiografia ya Wilaya hiyo wakulima wengi wanashindwa kufika hivyo wameona kuelekea msimu mpya wa Kilimo 2023/2024 watashusha maonesho hayo ngazi ya Wilaya na Kata.
Amesema, licha ya wilaya hiyo kutegemea kilimo katika uchumi wake bado wananchi wengi wanalima kilimo cha mazoea na kukosa mazao mengi na kushindwa kujikwamua kiuchumi.
“serikali inaweza kuleta umeme,maji,barabara,na vituo vya afya lakini kama tusipoboresha kipato cha mwananchi mmoja mmoja ni kazi bure dhamira yetu kila mwananchi awe na maisha bora,nyumba nzuri pamoja na kumiliki bima ya afya,” alisema Makame.