Scolastica Msewa – Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Godfrey Kasekenya amewataka Wakandarasi Wanawake kuungana, ili kuunganisha nguvu ya kuweza kutekeleza miradi mikubwa ya Ujenzi nchini.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wakandarasi Wanawake jijini Dar es Salaam, Injinia Kasekenya amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Wakandarasi wanawake wanaimarika na kutekeleza miradi mingi ya Serikali na hivyo kutoa fursa.
Amesema, Serikali itaendelea kutenga miradi ya ujenzi kwa ajili ya wakandarasi wanawake ili kuwawezesha wakandarasi hao kupata uzoefu, kukuza mitaji na kutoa fursa kwa Watanzania.
“Chapeni kazi kamilisheni miradi kwa wakati ili Serikali iwaamini na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kupata kazi nyingi,” amesema Eng. Kasekenya.
Naibu waziri huyo, amewataka wakandarasi wanawake kuwa waaminifu na waadilifu ili kuaminiwa na taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za kifedha.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake, Injinia Judith Odunga ameishukuru Serikali kwa namna inavyotoa vipaumbele vingi kwa wakandarasi wanawake na kusisitiza utaratibu huo ukiendelea uchumi kwa wakandarasi wanawake utakuwa na kuchochea maendeleo ya nchi.
Huo unakuwa ni mkutano Mkuu wa tatu kufanyika kwa wakandarasi Wanawake na hufanyika mara moja kwa mwaka ukilenga kuwakutanisha pamoja, ili kujadili changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi.