Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini – TARURA, Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmauel Ndyamkama amesema ataendelea kusimamia ubora wa kazi zinazofanyika katika Mkoa huo kwa kuzingatia matakwa ya mikataba inayosainiwa baina ya TARURA na Wakandarasi.

Hayo yamejiri wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Daraja la Ruhembe liliopo Kata ya Ruhembe Jimbo la Mikumi katika Wilaya ya Kilosa ambapo Ndyamkama amesema daraja hilo lenye urefu wa mita 40 limefikia asilimia 80 ya ujenzi wake.

Amesema, “Daraja hili kama linavyoonekana ni sehemu ya miradi inayotekelezwa katika mkoa huu, kuna baadhi ya watu wasio na nia njema wanaojaribu kupotosha juu ya jitihada hizi lakini kimsingi kazi hizi zinajionesha na ubora unazingatiwa.”

Mhandisi Ndyamkama ameongeza kuwa, “ TARURA Morogoro haitosita kuwachukulia hatua makandarasi na hata watumishi watakaobainika kuzorotesha ama kuhujumu kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara na kwamba atahakikisha lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa wananchi linafikiwa.”

Akiongea katika eneo hilo, mkazi wa Kata ya Ruhembe, Hassan Salum Mwaking’inda amesema ujenzi wa Daraja hilo utasaidia wananchi katika kuzifikia huduma za kijamii pamoja na kufanya biashara.

Ntibanzokiza, Kramo waitwa mezani Simba SC
Kasekenya awapa neno Wakandarasi Wanawake