Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu ametoa wito kwa Vijana Vilayani humo kujitokeza kwa wingi katika Kilimo cha Pamba, kwani ni moja ya fursa inayoweza kuwatoa kimaisha badala ya kujikita kwenye michezo ya Kamari.
Buswelu ametoa wito huo Oktoba 12,2023 wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Vikonge katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika soko la Vikonge na kusema zao la pamba limewatoa wengi kimaisha na Serikali hugharamia kuanzia mbegu, viatilifu na wataalamu wa utoaji wa elimu kwa Mkulima.
Amesema, pia wataalamu hao wanatakiwa kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi juu ya umuhimu wa zao hilo, ikiwemo kuwaorodhesha kwenye daftari wote wanaohitaji kulima Pamba msimu mpya wa Kilimo huku akiwakaribisha wananchi, Taasisi mbalimbali na wadau wa Kilimo kushiriki wiki ya Mwanakatavi inayotarajia kuanza Oktoba 25 – 31, 2023 katika Viwanja vya shule ya msingi Kashato Mpanda.
Wiki ya Mwanakatavi, ilianzishwa 2022 na Uongozi wa Mkoa wa Katavi ikilenga kuwakutanisha Wananchi na Wataalamu mbalimbali, ili waweze kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Kilimo, Utalii, Ufugaji, Biashara ambapo Mkuu wa Mkoa huwaongoza Wananchi na wadau kwenda kutalii Hifadhi ya Wanayama ya Taifa Katavi.