Mkurugenzi wa Kampuni ya PAF Promotion Entertainment, Godson Karigo amesema yupo kwenye hatua za mwisho za kumfikisha mahakamani Bondia Hassan Mwakinyo kwa kukiuka mkataba baina yao.
Karigo amesema mbali na mkataba wanalenga kulipwa fidia ya hasara waliyoipata baada ya Bondia huyo kugoma kupanda ulingoni Septemba 29, mwaka huu sambamba na kutoa maneno ya kashfa dhidi ya kampuni hiyo.
“Tunafanya taratibu za kukamilisha kulifikisha hili suala mahakamani, tunataka fidia ya kilichopotea na matusi tuliyotukanwa kurugenzi na kampuni nzima kuchafuliwa, maana ametuita sisi wababaishaji, tunadhulumu mabondia na mengi kama hayo,” amesema Karigo.
Aidha, Karigo hakuwa tayari kuweka wazi alipoulizwa kuhusiana na gharama ya fidia wanayokwenda kudai.
“Bado tunafanya hesabu kuhusu hiyo fidia, tutaeleza hesabu kamili ni ipi lakini kwa sasa bado tunaendelea na mchanganuo kisha tutaweka wazi baada ya pia kumaliza mchakato wa kesi ndani ya siku mbili tatu hizi,” amesema Karigo.
Karigo ameamua kufanya hivyo ikiwa ni siku tatu zimepita tangu Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kumfungia Mwakinyo kwa mwaka nmoja na faini ya Shilingi milioni moja kutokana na kutopanda ulingoni siku hiyo na kukiuka mkataba.