Baada ya Mlinda Lango wa Mtibwa Sugar, Mohamed Makaka kuanguka ghafla na kuzimia wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji ukiendelea, sasa rasmi nyota huyo amepona na yupo tayari kurejea mazoezini.

Baada ya kuanguka kwenye mchezo huo wa Septemba 15 na kumalizika kwa sare mabao ya 1-1, Makaka alipatiwa huduma ya kwanza kisha kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Nafasi yake ilichukuliwa na Razack Shekimweri, ambaye alidaka pia kwenye mechi mbili zilizofuata dhidi ya Singida Fountain Gate na Tanzania Prisons, ambazo zote Mtibwa ilipoteza.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Habib Kondo amesema hali ya Makaka inaendelea vizuri na muda wowote kuanzia leo Ijumaa (Oktoba 13) atajiunga na wachezaji wenzake katika mazoezi ya pamoja.

“Taarifa niliyopewa anaendelea vizuri na yupo tayari kuanza mazoezi. Ni kipa mzoefu na bora, hivyo ni habari njema kwetu na tunamuhitaji haraka ili kuendelea kujiandaa na mechi zijazo,” amesema Kondo aliyejiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akichuka mikoba ya Salum Mayanga.

Mtibwa Sugar inashika nafasi pili kutoka mkiani (15) kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imecheza mechi tano, ikipata sare mbili, huku ikichapwa tatu na kuambulia pointi mbili, sawa na Coastal Union inayoburuza mkia.

Mechi ijayo Mtibwa itakuwa nyumbani kuikaribisha Kagera Sugar, Oktoba 13, katika Uwanja Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Viongozi waliouza ekari 4,000 za Wizara wakamatwe - Kunenge
Ofisi ya Wakili Mkuu yaokoa Mabilioni ya Serikali