Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Miguel Angel Gamondi ametamba kuwa kurejea kwa baadhi ya wachezaji wake ambao walikosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Geita Gold FC kumekiongezea nguvu kikosi hiko kuelekea mchezo wao dhidi ya Azam FC.
Young Africans Oktoba 25, mwaka huu inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Kuelekea mchezo huo sehemu ya kikosi cha Young Africans cha wachezaji ambao hawajaitwa kwenye majukumu ya timu ya taifa kilirejea kambini juzi Jumatano (Oktoba 11), huku mastaa watatu waliokosa mchezo dhidi ya Geita Gold kwa sababu mbalimbali, ambao ni Jonas Mkude, Metacha Mnata na Farid Mussa wakiwa sehemu ya kikosi.
Kuhusu maandalizi ya kikosi chake, Gamondi amesema: “Tulitoa mapumziko mafupi baada ya mchezo wetu dhidi ya Geita Gold na licha ya kwamba tupo kwenye ratiba ya mashindano ya kimataifa lakini tumeanza kambi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Azam FC.
“Nafurahi kuona baadhi ya wachezaji ambao walikosa mchezo wetu dhidi ya Geita Gold wakiwa kambini, hii inatoa uwanda mpana ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam FC ambao ni wazi tunatarajia utakuwa mchezo mgumu.”