Mshambuliaji wa Geita Gold FC, Elias Maguri amezidi kuimarika baada ya kuanza kupona majeraha ya kifundo cha mguu (Enka).
Maguri aliumia katika dakika 15 za mwanzo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans, ambao timu yake ilifungwa kwa mabao 3-0.
Akizungumzia hali ya mchezaji huyo, Daktari wa Geita Gold, Abdallah Chuma amesema Maguri alipata maumivu kidogo ya kifundo cha mguu yaliyomfanya kushindwa kuendelea na mchezo, lakini kwa sasa anaendelea vizuri.
“Kweli Maguri aliumia na kushindwa kuendelea na mchezo ule, lakini si tatizo kubwa kwa sababu ni kifundo cha mguu (Enka), lakini ameanza kukaa sawa.
“Alikuwa anatembea vizuri baada ya mchezo kwahiyo maumivu sio makali sana kwake, bila shaka katika mchezo ujao atakuwepo kwenye kikosi.”
Juzi Alhamis (Oktoba 12), Geita Gold ilianza mazoezi rasmi baada ya kupumzika na sasa inajiandaa na mchezo wake ujao dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa katika Uwanja wa Nyankumbu, Oktoba 25.
Timu hiyo inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza mechi tano.