Boniface Gideon, – TANGA.

Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi 600 Bilioni na dola za Kimarekani Milioni 37.34 ambazo zingelipwa kwa wadaiwa endapo Serikali ingeshindwa kwenye mashauri hayo.

Hayo yamebainishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati akifungua kikao cha cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika Jijini Tanga.

Amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendesha mashauri 7,392 ambapo kati ya mashauri hayo 7,255 ni ya madai na 137 ni ya usuluhishi ambapo kati ya mashauri hayo 7,350 ni ya ndani ya nchi na 42 ni ya nje ya nchi.

“Kwa kipindi hicho hicho Ofisi hiyo imemaliza jumla ya mashauri 620 ambapo mashauri 579 yalimalizika kwa njia za kimahakama na mashauri 41 yalimalizika kwa njia ya majadiliano nje ya mahakama,” amesema Luhende.

Ameongeza kuwa wameshuhudia ongezeko la bajeti yao bungeni kwa ajili ya uendeshaji wa majukumu ya Serikali kuwatumikia wananchi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo katika kipindi hicho ofisi ya wakili mkuu wa Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ilifanikiwa kuongezewa bajeti kutoka zaidi ya Bilioni 12 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia zaidi ya Sh.Bilioni 17 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo ongezeko hilo ni asilimia 25.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Baraza, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Mulwambo alisema katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ofisi hiyo imejiwekea vipaumbele mbalimbali ni pamoja na kuendelea kuratibu, kusimamia na kuiwakilisha serikali na taasisi zake katika kuendesha mashauri ya madai yanayofunguliwa dhidi ya Serikali kwenye mahakama au mabaraza mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema pia wataendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ikiwemo mafunzo ya kibobevu katika maeneo maalumu ikiwemo ya sekta ya mafuta na gesi pamoja na usuhuluhi wa kimataifa kuimarisha ofisi za mkoa na hivi sasa wanaendelea kufungua ofisi nyengine mkoani Manyara.

Mohamed Makaka yu njiani Mtibwa Sugar
Jina la Jorginho mezani FC Barcelona