Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameutaka Mgodi wa Singida Gold Mine kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopo ndani ya eneo la leseni, ambao walikuwa bado hawajalipwa.
Mavunde ameyasema hayo mara baada ya kutembelea Mgodi huo uliopo Wilayani Ikungi na kuongeza kuwa mgodi huo umetimiza masharti ya leseni ya uchimbaji vyema, hivyo ni muhimu kuharakisha ulipaji wa fidia kwa Wananchi.
Amesema, “niwahimize kuharakisha suala la fidia kwa wananchi ambao bado, hii itawasaidia nyie kufanya shughuli zenu bila malalamiko ya wananchi wa maeneo yanayowazunguka, na kwa kuwa wamebaki wachache naamini halitachukua muda mrefu sana.”
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Singida Gold Mine, George Kondela amesema kuwa tayari Mgodi umewalipa fidia ya ardhi wananchi 236 na kuwajengea nyumba wananchi 12, na kwamba wanashughulikia fidia ya ardhi kwa wananchi 53 waliosalia na nyumba za wananchi 10.