Imefahamika kuwa Sir Jim Ratcliffe amekubali dili la kununua hisa asilimia 25 za Manchester United baada ya Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kutwaa nafasi hiyo.
Sheikh Jassim alikuwa akitafuta kutwaa klabu hiyo kwa asilimia 100, akitoa ofa ya kulipa takriban Pauni Bilioni tano kuchukua udhibiti wa United na pia kuashiria nia ya kulipa madeni ya Pauni Bilioni Moja ya klabu hiyo.
Hata hivyo, familia ya Glazers inayoimiliki klabu hiyo wanaithamini klabu hiyo juu zaidi, labda hadi Pauni Bilioni 10, na vyanzo vimethibitisha kwamba, Sheikh Jassim alijiondoa kwenye mchakato huo baada ya kukataa kuongeza ofa yake ya hivi karibuni.
Badala yake, makubaliano yamefikiwa na Ratcliffe, ambaye anatazamiwa kupata umiliki wa klabu hiyo kwa asilimia 25.
Ratcliffe anatumaini kupata umiliki kamili wa klabu katika siku zijazo, lakini yuko tayari kuanza na dau la hisa chache ambalo litaiwezesha familia ya Glazers kubakia kwenye umiliki wa asilimia kubwa pale Old Trafford kwa sasa.
The Glazers walikuwa wakisita kuiuza United kwa bei iliyo chini ya bei waliyotakiwa na kumekuwa na sintofahamu kwa muda mrefu kama dili lolote lingekubaliwa huku mazungumzo yakichukua karibu mwaka mmoja.
Lakini Ratcliffe, ambaye ofa yake kwa United ilithaminiwa zaidi na kabu hiyo kuliko ile ya Sheikh Jassim, amekubali kuchukua mbinu polepole zaidi ya kuichukua na ameweza kuwaridhisha familia ya Glazers.