Watu wanne Wafanyabiashara wanaoishi jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na mashitaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Shilingi 592.3 Milioni kwa kutoa risiti zisizo halali.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa Mahakamani na jopo la Mawakili wa Serikali wanne wakiongozwa na Wakili Mwandamizi, Grolia Mwenda imewataja washitakiwa hao kuwa ni Salum Mbegu (38), Hamad Hamad, Baraka Ntikula (37) na Peter Ntikula (27).
Inadaiwa kuwa, kati ya mwaka 2018 na Oktoba 3, 2023, huko Buguruni Kisiwani Wilaya ya Ilala, washtakiwa kwa lengo la kujipatia faida, waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia mashine ya EFD kuharibu mfumo, kumdanganya Kamishna na kutoa risiti zisizo halali.
Aidha, katika tarehe hizo pia washitakiwa hao walitumia mashine za EFD kwa lengo la kupotosha mfumo kwa kutoa risiti zisizo halali na kuziingiza kwenye mfumo wa TRA na kusababisha Mamlaka hiyo kudaiwa kodi ya ongezeko La Thamani (VAT) ya Sh 592,336,714.
Kwa pamoja wanadaiwa kutoa risiti bandia za EFD kwa nia ya kumdanganya kamishna na walipa kodi kudai kodi ya ongezeko La thamani (VAT) kinyume cha Sheria ambapo katika shtaka la nne ilidaiwa kuwa Oktoba 3, 2023 washitakiwa Mbegu, Ntiluka na Baraka, Walikutwa na mashine tano za EFD ambazo walizipata kinyume cha Sheria.
Mwenda ambaye alisaidiana kusoma mashtaka hayo dhidi ya washtakiwa na Mawakili wa Serikali Upendo Mono, Medalakini Emmanuel na Hauni Chilamula, Mbele ya Hakimu Mfawidhi, Susan Kihawa aliendelea kudai kuwa, katika shtaka la Utakatishaji fedha washitakiwa wote wanadaiwa kuhusika kutoa muamala wa Sh Milioni 592.3 Wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu.
Mashtaka mengine yanayowakabili washtakiwa ni Kuongoza genge la uhalifu, kutumia mashine za Kielektroniki za EFD kwa lengo la kuharibu mfumo na kumdanganya Kamishna, kutoa risiti zisizo halali za EFD na kukutwa na mali ya wizi au iliyopatikana kinyume cha sheria.
Hata hivyo washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo na wamerudishwa rumande kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu ambapo kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 30, 2023 itakapo tajwa tena.