Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeishauri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira, kupanua wigo wa fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi.

Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo cha kupokea na kujadili utendaji kazi wa kitengo hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq, amesema pamoja na juhudi za serikali kufungua fursa za ajira kuna umuhimu wa kuhamasisha watanzania kuchangamkia fursa za ajira nje ya nchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA), Bungeni, Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi wa Ofisi, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako naye ameahidi kufanyia kazi maoni ya kamati huku akimshukuru Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua ambazo amezichukua za kukuza uwekezaji nchini na kufungua fursa za ajira kwa watanzania.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Patrobas Katambi, amewahimiza watanzania wanaotaka kufanya kazi nje ya nchi kufuata utaratibu unaotambulika na serikali ili iwe rahisi kusaidiwa wanapopata changamoto.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema kitengo hicho kimetokana na kufutwa kwa Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) na majukumu yake kuunganishwa chini ya Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi.

Serikali yahimiza juhudi uchumi Kidigitali Wanawake, Vijana
Ben White aitamanisha Manchester City