Kocha Mkuu wa Brazil, Fernando Diniz amesema Neymar  ni mmoja wa wachezaji wakubwa katika historia ya mchezo wa soka baada ya nyota huyo kukosolewa hivi karibuni.

Neymar alipigwa na mfuko wa bisi kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya timu hiyo kutoka sare ya bao 1-1 na Venezuela nyumbani na Diniz kushutumu tukio hilo.

Neymar alikosolewa na mashabiki na vyombo vya habari vya nchi hiyo kwa kucheza chini ya kiwango.

“Hakuna kocha duniani anayeweza kumkataa Neymar kutokana na njaa ya kupata mafanikio aliyonayo,” alisema Diniz.

“Mara nyingine tena dhidi ya Venezuela alitoa pasi iliyozaa bao. Tayari nilishasema Neymar ni mmoja wa wachezaji katika historia ya soka la Brazil na dunia kwa ujumla.”

Neymar, aliyefikisha umri wa miaka 31, mwezi uliopita alivuka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye timu ya taifa ya Brazil iliyowekwa na Pele ambapo amefunga mabao 79 katika mechi 125 alizoichezea timu hiyo.

“Kitu kimoja cha kusema kuhusu Neymar ni namba zake, ni wa kwanza katika kila eneo kama mshambuliaji,” alisema Diniz.

“Wa kwanza kwa kufunga mabao mengi, kushiriki kwenye kupatikana kwa mabao, kukokota mpira…namba zake zinajieleza kwanini ni mchezaji muhimu hapa.”

Nyota huyo anayekipiga kwenye klabu ya A Hilal alichukizwa na tukio hilo la mashabiki wa Brazil kumrushia mfuko wa bisi.

“Siji hapa kufanya starehe au kufanya matembezi, nakuja hapa kufanya kile ninachokipenda zaidi, ambacho ni kucheza soka,” alisema Neymar

Rais Samia azungumza na Wafanyabiashara Nzega
Ally Mayay amkumbusha Karia na TFF yake