Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri Serikali kuweka kipaumbele katika kusambaza Vituo vya Nishati ya Gesi Iliyoshindiliwa (CNG) inayotumika katika kuendesha mitambo na magari nchini ili kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa mafuta pale zinapotokea.
Ushauri huo umetolewa Oktoba 18, 2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David wakati Kamati hiyo ilipopokea taarifa ya Wizara ya Nishati, kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kuanzisha vituo hivyo.
“Tunashauri Serikali iweke kipaumbele katika matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na matumizi mengine ili Watanzania waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi,” amesema Mwenyekiti wa Kamati, Mathayo David.
Katika hatua nyingine, Mathayo ameipongeza Serikali kwa mikakati mizuri ya uanzishwaji wa karakana za kubadili mifumo ya matumizi kutoka kwenye mafuta na kwenda kwenye gesi asilia kwenye magari hali inayochochea matumizi ya gesi asilia nchini kwa wingi.
“Uwepo wa karakana hizi kwa wingi utarahisisha utoaji wa huduma za ubadilishaji mifumo na ukarabati wa hitilafu kwa muda mfupi na karakana hizi zitumie teknolojia ya kisasa wakati wa kubadili magari na mitambo,” ameeleza Mhe. Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imepokea ushauri wote uliotolewa na kamati ili kuweza kuboresha Sekta ya Nishati nchini na kudai kuwa Wizara imedhamiria kuchochea matumizi ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa kwa maeneo pia yaliyo mbali na mtandao wa mabomba pamoja na matumizi ya gesi hiyo kwenye magari kwa kuwa na vituo vingi vya kujazia gesi kwenye magari.
Viongozi mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga na Watendaji kutoka Wizara na Taasisi.