Wizara ya mambo ya ndani imesema shambulizi la anga la Israel limeuwa na kujeruhi idadi kubwa ya watu waliokuwa wamepata hifadhi katika eneo la Kanisa la Mtakatifu Porphyrius huko Gaza, katika eneo hilo lenye mzingiro la Wapalestina.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya Habari, vimesema shambulio hilo lilionekana kulenga lango lililokuwa karibu na mahali pa ibada, ambapo wakazi wengi wa Gaza Wakristo na Waislamu walikuwa wamepata hifadhi wakati vita vilipokuwa vinaendelea eneo hilo.
Kanisa hilo, lililojengwa miaka ya 1150, ni kanisa linalotumiwa hadi leo huko Gaza kanisa hilo limekuwa mahali pa hifadhi kwa watu wa dini mbalimbali kwa vizazi kadhaa.
“Kulenga makanisa na taasisi zao, pamoja na mahali wanapotoa hifadhi kwa raia wasio na hatia, hasa watoto na wanawake waliopoteza makazi yao kutokana na mashambulizi ya Israel kwenye maeneo ya makazi katika kipindi cha siku 13 zilizopita, ni uhalifu wa kivita usioweza kupuuzwa,” ilisema taarifa hiyo.
Gaza imeshambuliwa kwa mfululizo na mashambulizi ya Israel kufuatia shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7, ambalo Israel inasema liliua angalau watu 1,400, wengi wao raia.
Kampeni ya Israel tangu wakati huo imesababisha vifo vya Wapalestina 3,785 katika Ukanda wa Gaza, wengi wao wakiwa raia, kulingana na wizara ya afya ya Hamas.