Kiungo kutoka DR Congo Yannick Bangala amerejea uwanjani baada ya kupona majeraha aliyoyapata Oktoba 3, mwaka huu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na huenda akacheza mechi ijayo kati ya Azam FC dhidi ya Young Africans.
Kitendo cha kupona kwa Kiungo huyo kimekuwa kicheko kwa Benchi la Ufundi la Azam Fc linaloongozwa na Kocha kutoka nchini Senegal Youssouph Dabo, kwani atakuwa na maamuzi ya kumtumia kwenye mchezo wa keshokutwa Jumatatu (Oktoba 23).
Bangala alichanika nyama za paja na kukaa nje ya uwanja kwa majuma mawili, lakini hivi sasa yuko tayari kucheza hivyo analisikilizia benchi la ufundi la timu hiyo kumpa nafasi.
Kocha mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema kupona kwa Bangala ni faraja kwao kwani ni mchezaji mzuri na pia mzoefu wa mechi kubwa.
“Tunafurahi amerejea, ataongeza kitu kwenye kikosi chetu kwani anauzoefu wa kutosha,” amesema Dabo.
“Bado tunajiandaa na mechi ijayo, kumpanga au kutompanga itategemea ataonyesha nini hadi siku ya mwisho ya mazoezi. Tusubiri tutaona.”
Bangala alijiunga na Azam FC msimu huu akitokea Young Africans ambayo aliichezea kwa misimu miwili huku msimu wake wa kwanza 2021/2022 akiibuka kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu (MVP).
Azam FC itakutana na Young Africans ikiwa na kumbukumbu ya kutoshinda mechi hata moja kati ya tano zilizopita timu hizo zilipokutana ikiwa imetoa sare mbili na kupoteza tatu.