Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaasa wachimbaji wadogo kuachana na vitendo vya utoroshaji madini.
Rais Samia ametoa wito huo wakati akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa mitambo ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo pamoja na mitambo ya Shirika la Madini la Taifa – STAMICO.
Amesema, wachimbaji wadogo hawana budi kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuhakikisha kuwa wanauza madini yao katika viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu, ili kuchochea uchumi wa viwanda.
Aidha, Rais Samia pia amewataka wachimbaji hao kufuata sheria, kanuni na miongozo
iliyopo katika sekta ya madini ili kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinawanufaisha Wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi Nchini.
Amewahakikishia wachimbaji wadogo wa madini nchini kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya uchimbaji pamoja na biashara ya madini, ili waweze kuchangia kwenye uchumi wa taifa.
Katika hatua hizi za mwanzo za utekelezaji wa mpango huo, mitambo mitano yenye
thamani ya shilingi bilioni 2.73 imezinduliwa ambayo iko tayari kufanya kazi katika
maeneo ya wachimbaji wadogo hapa nchini.