Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema amewaona Al Ahly na ataiandaa kikamilifu timu yake kukabiliana na miamba hiyo ya soka Barani Afrika.

Gamondi alikuwa ni mmoja wa walioushuhudia mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) Uwanja wa Benjamin Mkapa kati ya Simba SC na Al Ahly na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Kocha huyo raia wa Argentina amesema hana mengi ya kuzungumza kuhusiana na wapinzani wake hao isipokuwa atatumia siku zilizobaki kukiimarisha kikosi chake ili kukabiliana nao katika mechi zote mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika watakazokutana.

“Nimewaona Al Ahly ni timu kubwa na bora Afrika, wana wachezaji wenye uwezo na uzoefu mkubwa lakini vipo vitu nimeviona tunakwenda kuvifanyia kazi kwa ajili ya kuvitumia kwenye mchezo wetu wa hatua ya makundi,” amesema Gamondi

Gamondi amesema mpira ni mchezo wa mbinu ambao unabadilika kila kukicha hivyo ni vigumu kuyafanyia kazi moja kwa moja mapungufu waliyoyaona kwa Al Ahly kwa sababu wanaweza kuja tofauti na kuwapa wakati mgumu.

Amesema atakachofanya ni kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya kushindana na timu kubwa Afrika na siyo kufuata moja kwa moja kile alichokiona kwenye mchezo wa Ijumaa (Oktoba 20).

Mbali na Al Ahly timu nyingine zilizopo kwenye kundi la Young Africans ni CR Belouzdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Tumieni fursa za uwekezaji, toeni ushirikiano - Majaliwa
Ntibazonkiza: Tutapambana hadi tone la mwisho