Baada ya Kocha Cedric Kaze kujiuzulu kukinoa kikosi cha Namungo FC, uongozi wa klabu hiyo umesema timu itakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Denis Kitambi, ambaye atasimamia mechi ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC wakati ukisaka kocha mwingine.
Awali, Kitambi alikuwapo kwenye benchi hilo kama kocha msaidizi akisaldiana na Kaze kabla ya kujiuzulu kwa sababu ya mwenendo mbaya katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa Namungo FC, Namlia Kindamba, amesema baada ya kuona taarifa za kujiuzulu kwa Kaze uongozi umeamua timu kuendelea kubaki chini ya Kitambi akishirikiana na Kocha wa viungo, Shadrack Nsajigwa, hadi hapo watakapofanya maamuzi mengine.
Amesema kutokana na kujiuzulu kwa Kaze, hawatapata athari yoyote ya maandalizi ya mchezo wao ujao dhidi ya Azam FC, na wanaimani kubwa ya kufanya vizuri wakiwa na Kitambi
“Tunaheshimu maamuzi ya Kaze kujiuzulu, maisha mengine yanaendelea na kikosi kitaondoka leo, kuelekea Dar es salaam kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC.
“Kocha Kitambi na Nsajigwa wataendelea majukumu ninaimani tutafanya vizuri kwenye mechi yetu dhidi ya Azam FC kama ilivyo kwa msimu uliopita kuchukua alama na kwenye tatu dimba la Azam FC,” amesema Kindamba.
Ameongeza kuwa wanaingia Dar es salaam mapema kwa lengo la kupata siku mbili za kufanya mazoezi kabla ya kukutana na Azam FC.
Amesema wanatambua haitakuwa mechi rahisi kwa sababu ya ubora wa wapinzani wao hao na ugumu wa ligi kwa msimu huu, lakini wamejipanga kupambana kutafuta pointi katika kila mchezo ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa Ligi hiyo.
Namungo FC inashika nafasi ya l4 kutoka chini ikicheza michezo sita ikipoteza mitatu na sare tatu hajashida mechi hata moja.