Shughuli ya kwanza kwa kocha mpya wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, itaanza kesho Alhamis (Oktoba 26) atakapoiongoza timu yake kwenye mechi dhidi ya Geita Gold, Uwanja wao wa Manungu Complex uliopo Turiani mkoani Morogoro.

Mtibwa Sugar ilimtangaza rasmi kocha huyo juzi Jumatatu (Oktoba 23) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Habib Kondo aliyeoneshwa mlango wa kutokea baada ya matokeo mabaya katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katwila, ambaye ni Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, alijiuzulu kwenye timu yake aliyokuwa akifundisha zamani, Ihefu FC, ikiwa ni siku chache baada ya kuifunga Young Africans mabao 2-1 Oktoba 4, na kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Ihefu FC, Oktoba 7, mwaka huu.

Wakati anaondoka Ihefu, tayari kulikuwa na minongono ya kuelekea Mtibwa Sugar kabla hata ya kutangazwa rasmi.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thobias Kifaru, amesema wana uhakika kikosi chao kitabadilika kiuchezaji kutokana na mbinu za mwalimu huyo ambaye anajua falsafa ya klabu hiyo.

“Amerudi nyumbani, hatuna wasiwasi naye, alikuwa straika wetu kwa hiyo anaijua Mtibwa Sugra nje na ndani, naamini atatusaidia kwenye kipindi hiki kigumu,” amesema Kifaru.

Zuberi tayari ameanza kazi ya kukinoa kikosi hicho na kesho Alhamis (Oktoba 26) ataisimamia timu hiyo kwa mara ya kwanza wakati ikicheza nyumbani dhidi ya Geita Gold.

Kazi aliyonayo ni kuhakikisha inapata ushindi wa kwanza, kwani mpaka sasa licha ya kuburuza mkia, haijashinda mechi yoyote ya Ligi Kuu ikicheza michezo sita, sare mbili na kupoteza nne, ikiweka rekodi mbaya msimu huu ya kupoteza mechi tatu nyumbani kati ya nne ilizocheza.

Waziri Mavunde amshukuru Aziz Ki
Mradi JHHPP uanze mapema - Rais Dkt. Samia