Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amewashauri wafugaji Mkoani Katavi kufuga kisasa badala ya kufuga makundi makubwa ya mifugo yenye tija ndogo.
Akihutubia wananchi waliojitokeza katika siku ya pili ya Tamasha la Wiki ya Mwanakatavi, Mnyeti amesema kuwa wafugaji wanapaswa kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo michache iliyoboreshwa ambayo itakuwa na faida kwa mfugaji.
‘Amesema, ‘kupitia Wizara hii tunaendelea kuhimiza ufugaji wa kisasa, Katavi ni miongoni mwa maeneo ambayo yana ufugaji wa kiholela ufugaji usiokuwa na tija ufugaji ambao ng’ombe kukicha hawajui wanaenda kula wapi.”
Aidha, Mnyeti amesema kumekuwa na changamoto ya ufugaji wa kuhamahama kwa baadhi ya Wafugaji hali ambayo huwafanya waione kazi ya ufugaji kama mzigo na baadhi yao kukataa tama na ufugaji.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali kupitia Wizara Mifugo na Uvuvi imeendelea kuboresha Miundombinu ya ufugaji kwa kujenga Malambo na Majosho, kama sehemu ya kutambua mchango wa sekta ya mifugo katika kuongeza pato la Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya Ufugaji katika Mkoa wa Katavi imeleta zaidi ya Bilioni Moja kwa ajili ya kujenga Bwawa la kunyweshea Mifugo.
Kuhusu migogro ya Wakulima na Wafugaji Buswelu amesema Halmashauri zimeendelea kufanya mpango wa Matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya kulima na kufuga, ambapo mpaka sasa zaidi ya hekta 16,000 zimetengwa kwa ajili ya maeneo hayo.
Wiki ya Mwanakatavi leo Oktoba 27, 2023 inaingia siku ya tatu katika viwanja vya CCM Azimio mjini Mpanda, kwa kukutanisha Taasisi za Umma na Binafsi kwa lengo la kutangaza bidhaa zinazopatikana Mkoa wa Katavi na fursa zilizopo.