Scolastica Msewa – Dar es Salaam.

Wajasiriamali wametakiwa kutumia vizuri maonyesho mbalimbali yanayoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni – BRELA, kutangaza bidhaa mbalimbali wanazozalisha, ili wapate masoko na kujipatia kipato.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mkoani Dar es Salaam, Edward Mpogolo wakati wa ziara yake ya kutembelea mabanda ya biashara za wajasiriamali katika viwanja vya Mlimani city, katika maonesho ya kwanza ya Wakala wa Usajili wa biashara na Leseni BRELA na Wadau wake, ili kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na wajasiriamali nchini.

Amesema, “wito wangu kwa Wajasiriamali ni kwamba watumie Maonyesho haya vizuri kwa kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali wanazozalisha badala ya kufurahia tu kuuza bidhaa zao.”

Aidha, Mpogolo pia amewashukuru wajasiriamali kwa kuitikia mwito wa BRELA katika maonesho yao kwa kushirikisha Wadau mbalimbali wa uzalishaji na watoa huduma, kwa kwenda kuonesha shughuli na bidhaa zao mbalimbali wanazozalisha nchini.

Amewataka pia BRELA na Taasisi mbalimbali wezeshi za wajasiriamali kuendelea kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali wanazozalishwa na wajasiriamali nchini kwani wengi wao hukopa mitaji katika mabanki na taasisi mbalimbali za fedha ili wapate faida kupitia ujasiriamali wao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo amewataka Wajasiriamali ambao bado hawajasajili biashara zao na kupata Leseni za BRELA wakasajili, ili waweze kufanya biashara zao kwa kupata uhalali na kuaminiwa sokoni.

“Wapo watu wanaona BRELA kama Polisi vile niwatoe hofu BRELA wanatoa elimu, ushauri na wanamsaidia Mjasiriamali kukua katika biashara zake BRELA wanasajili, wanamsaidia Mjasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zao ili kuwakuza kwa namna moja ama nyingine,” amesema Halima.

Duke Abuya aichimba mkwara Young Africans
Wiki ya Mwanakatavi: Serikali yawapa somo Wafugaji