Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amemwagia sifa mshanbuliaji wake, Eddie Nketiah kwa kiwango alichokionyesha juzi Jumamosi (Oktoba 28) na kuisaidia timu hiyo kushinda mabao 5-0 dhidi ya Sheffield United.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya England uliopigwa katika Uwanja wa Emirates, Nketiah alibuka mchezaji bora wa mechi baada ya kufunga mabao matatu ‘hat-trick’, kabla ya Takehiro Tomiyasu na Fabio Vieira kukamilisha ushindi wa 5-0.
Nketiah aliongoza safu ya ushambuliaji ya Arsenal katika mchezo huo kufuatia nyota Gabriel Jesus kuuguza jeraha la misuli ya paja.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania amempongeza Mshambuliaji huyo na kusema nyota huyo ni mchezaji wa daraja la juu.
“Kwangu mimi, yeye yupo daraja la juu. Ameanza katika mechi nane kati ya 10 za Ligi Kuu msimu huu. Hiyo inakuambia ni kwa kiasi gani tunamuamini na ana umuhimu gani katika timu.
“Nina furaha sana juu yake, mchezaji kutoka akademi (ya Arsenal) kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika Ligi Kuu ya England” amesema.
Kocha huyo ameongeza kuwa, nyota huyo anapaswa kufurahia wakati bora alionao hivi sasa.
“Anastahili kabisa hilo na naamini kuna mengi zaidi yanakuja. Ana jicho la goli,” amesema.
Pia, Arteta amesema nyota huyo anahitaji muda wa kutosha na nafasi ili kuendelea kufunga mabao mengi.
Baada ya mchezo wa juzi Jumamosi (Oktoba 28), kikosi cha Arsenal keshokutwa Jumatano (Novemba Mosi) kitavaana na West Ham katika Robo Fainali ya EFL.