Benchi la Ufundi la Young Africans, limeweka wazi kuwa, malengo yao ni kupata ushindi kwenye mechi zote watakazocheza ikiwa ni pamoja na ule dhidi ya Simba SC ili kufikia malengo ya kuendeleza kasi yao.
Jumapili (Novemba 05), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Young Africans inatarajiwa kumenyana na Simba SC ikiwa ni Kariakoo Dabi.
Ikumbukwe kwamba kwenye mechi mbili walizokutana langoni alipoanza Ally Salim mastaa wao walikwama kumtungua ndani ya dakika 90.
Kuna uwezekano mkubwa langoni kwa mara nyingine akaanza Salim kutokana na Aishi Manula kutokuwa fiti licha ya kuanza mazoezi na makipa wengine ikiwa ni pamoja na Ayoub Lakred ambaye hakupata nafasi kwenye mechi zilizopita.
Ilikuwa ni kwenye mchezo wa ligi ubao wa Uwanja wa Benjamin Mkapa uliposoma Simba 2-0 Young Africans, zama za Nasreddine Nabi kwa mabao ya Henock Inonga na Kibu Denis na ule wa Ngao ya Jamii Uwanja wa Mkwakwani, Young Africans 0-0 Simba SC, ushindi ulipatikana kwa Penati, Young Africans 1-3 Simba SC.
Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Young Africans, amesema kuwa kikubwa ambacho kinatakiwa kwenye mechi watakazocheza ni kushinda bila kujali aina ya mpinzani watakayekutana naye.
“Malengo yetu ni kushinda kwenye mechi ambazo tunacheza bila kujali ni aina gani ya mpinzani ambaye tunakutana naye.
“Tunatambua kwamba ligi ina ushindani mkubwa nasi tunajipanga kwa ajili ya hilo ili kupata pointi tatu na ili uzipate ni muhimu kufunga,” amesema Gamondi.